Lugha na mitazamo ya wazungumzaji wa kĩndia na kĩgĩchũgũ Kuhusu utambulisho wao wa kijamii

No Thumbnail Available

Date

2023-03

Journal Title

Journal ISSN

Volume Title

Publisher

Egerton University

Abstract

Mawasiliano ni mchakato unaohusisha uhawilishaji wa ujumbe pamoja na uundaji na udumishaji wa utambulisho baina ya wazungumzaji. Katika maingiliano, binadamu hujaribu kuunda, kuendeleza na kudumisha utambulisho wake wa kijamii kupitia lugha. Utafiti huu ulinuia kuchunguza maingiliano na mahusiano baina ya wazungumzaji wa lahaja za Kĩndia na Kĩgĩchũgũ na wazungumzaji wengine wa Kikikuyu kimazungumzo. Utafiti ulitilia maanani jinsi wazungumzaji wa lahaja za Kĩndia na Kĩgĩchũgũ wanavyounda na kuendeleza utambulisho wao wa kijamii katika hali ya mtagusano wa kilahaja. Binadamu huashiria utambulisho wao kupitia lugha hasa kwa jinsi wanavyoteua matumizi ya misimbo mbalimbali. Malengo matatu mahususi yaliongoza utafiti huu; kubainisha mitazamo ya wazungumzaji wa Kĩndia na Kĩgĩchũgũ kuhusu utambulisho wao. Pili, kutathmini sababu za kujitambulisha na jamii ya Wakikuyu. Tatu, kuchanganua michakato ya kiisimu ya kiukaribiano ambayo wazungumzaji wa Kĩndia na Kĩgĩchũgũ huhusisha katika uundaji wa utambulisho wa kijamii. Utafiti uliongozwa na nadharia mbili; nadharia ya Utambulisho wa Kijamii na nadharia ya Ukaribiano wa Kimawasiliano. Utafiti huu ulikuwa wa kithamano na ulizingatia muundo wa kimaelezo. Mbinu za mahojiano, na uchunguzi shiriki katika miktadha isiyo rasmi zilitumika katika ukusanyaji wa data. Sampuli ya kimaksudi ilitumika kuteua mshiriki mmoja ambaye alisaidia katika uteuzi wa washiriki 48 kupitia sampuli tajwa. Uchanganuzi na uchambuzi wa data ulikuwa wa kimaelezo na ulihusisha uandaaji wa tunukuzi ambazo zilitafsiriwa kwa Kiswahili na baadaye kuwasilishwa kwa maelezo na majedwali. Matokeo ya utafiti yalidhihirisha kuwa watafitiwa walikuwa na mitazamo chanya na hasi kuhusu utambulisho wao wa kijamii. Asilimia sabini ya watafitiwa walikuwa na mtazamo kuwa vibainishi vya utamaduni, desturi, mila, historia na lugha sawa huwapa utambulisho wao kama wanajamii wa jamiilugha ya Wakikuyu. Hata hivyo, asilimia ishirini na saba ya watafitiwa walikuwa na mtazamo kuwa ‘Gĩkĩrĩnyaga’ kama lugha yao huwapa utambulisho tofauti kama Wakĩrĩnyaga na hawaoni haja ya kubadili usemi. Watafitiwa waliendeleza maafikiano kwa madhumuni ya kufanikisha mawasiliano na kukubalika. Hata hivyo, walisistiza mwachano ili kudumisha lahaja zao ambazo walikuwa na mtazamo kuwa zinaweza kufifia. Utafiti huu umetoa maarifa kuhusu utambulisho wa kijamii na pia mchango katika isimujamii kuhusu jinsi matumizi ya lugha huendeleza utambulisho wa mtumiaji lugha.

Description

Keywords

Citation