Abstract:
Baadhi ya nomino za Kiwanga hubadili maumbo kutoka umbo-ndani hadi umbo-nje inapokuzwa au kudunishwa. Mabadiliko haya husababishwa na mifanyiko ya kimofofonolojia kutokana na uamilifu wa mofu {ku-/mi-} au {xa-/ru-}. Mifanyiko hii hudhihirika mofu za ukuzaji na udunishaji zinapoathiriana na segementi za mizizi ya nomino. Tasnifu ya utafiti huu ilijengwa kwa mada; Mifanyiko ya kimofofonolojia ya ukuzaji na udunishaji nomino za Kiwanga. Lengo la utafiti huu ulikuwa kuonyesha hatua za ukokotezwaji wa maumbo-ndani hadi maumbo-nje ya nomino. Hatua hizi zilibainishwa kwa mofu maalum kuathiriana na segmenti za mizizi, mifanyiko ya kimofofonolojia kukokotoa mabadiliko ya maumbo ya nomino husika na kanuni za kifonolojia kuongoza mifanyiko husika. Mabadiliko ya maumbo ya nomino yalifasiriwa kwa kuongozwa na mihimili ya nadharia ya Fonolojia Umbo-upeo. Mihimili hii ni pamoja na; kihimili cha uzalishi, masharti-zuizi na tathmini. Deta ya utafiti huu ilikuwa nomino sitini na tano za Kiwanga. Nomino hizi zilitokana na mijadala na mahojiano ya kimakundi kuhusu mada kama vile; Kilimo, Ufugaji, Vifaa vya matumizi ya nyumbani, Mazingira, Utalii, Sehemu za mwili nk. Makundi kumi na matatu ya washiriki kumi kumi yalifanya mazungungumzo ya kawaida ili kutaja nomino kumi kwa kila kikundi. Takribani nomino mia moja na thelathini zilichanganuliwa huku nomino zenye sifa maalum za kifonolojia zikizingatiwa. Nyingi zilikuwa na mshabaha wa sifa za kifonolojia na hivyo kuchujwa na kusalia na idadi ya nomino sitini na tano. Deta hiyo iliwasilisha nomino tofauti tofauti zenye sifa maalum za kifonolojia kwa ajili ya uchanganuzi ili kujibu maswali ya utafiti. Matokeo ya utafiti huu yanatarajiwa kukitambulisha Kiwanga kama lugha ya kurejelewa na wanaisimu-linganishi wanapotafitia mifanyiko ya kimofofonolojia katika lugha za Kibantu. Utafiti huu uliendeshwa katika Jimbo dogo la Matungu iliyoko Jimbo la Kakamega nchini Kenya.